ALIYEUA MWIZI AHUKUMIWA KUNYONGWA MPAKA KUFA

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala ya Iringa imemuhukumu Elia Martine Ngaile @ Rasta (54) kunyongwa mpaka kufa baada ya kupatikana na hatia ya kosa la Mauaji ya Luca Pascal Mang’wata.
Hukumu hiyo imetolewa tarehe 7 Machi 2025 na Mhe. Jaji Angaza Mwipopo baada ya kusikiliza mashahidi wanne (4) wa upande wa jamhuri pamoja na vielelezo viwili (2) na kujiridhisha kwamba kesi upande wa Jamhuri imethibitishwa pasipo kuacha shaka.
Katika kesi hiyo ya Kikao cha Jinai Na. 26195 ya mwaka 2024, Bw. Elia ambaye ni mkazi wa kijiji cha Ndiwili, wilaya ya Kilolo mkoa wa Iringa alikuwa anakabiliwa na shtaka la Mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu, (Sura ya 16 Rejeo la mwaka 2022.)
Mshtakiwa alitenda kosa hilo tarehe 21 Mei, 2024 katika kijiji cha Lundamatwe, kitongoji cha Kibati, Wilaya ya Kilolo ambapo inadaiwa mshtakiwa alikuwa akitafuta mwizi wa ng’ombe wanne (4) na alifanikiwa kumkamata marehemu na kumfungia katika kilabu cha pombe na marehemu alipotaka kukimbia alimkamata na kumkata na panga kichwani, mkononi na miguuni. Kitendo hicho kilisababisha marehemu kuvunjika miguu yote miwili na fuvu la kichwa kuwa wazi pamoja na ubongo kuonekana. Majeruhi alipelekwa hospitali kwa matibabu hatimae alifikwa na umauti akiwa anapatiwa matibabu hospitali ya Rufaa Iringa.
Kesi hii imeendeshwa na Mawakili wa Serikali wawili kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ambao ni Muzzna Mfinanga akisaidiana akisaidiana na Majid Matitu.