WATUMISHI WAASWA KUYAENZI MAZURI YA MAREHEMU MAUGGO
Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mhe. Juma Chikoka amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi kwenye mazishi ya Marehemu Peter Mauggo aliyekuwa Mtumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma yaliyofanyika tarehe 24 Oktoba, 2024 katika kijiji cha Kurugee, Majita wilaya ya Musoma Mkoani Mara.
Akitoa salamu za pole za Mhe. Kanali Mtambi, Mhe. Mkuu wa Wilaya amesema Mhe. Mkuu wa Mkoa ametoa pole kwa wafiwa wote, ndugu, jamaa na marafiki na kuwasihi kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo na waendelee kumwombea Marehemu Peter Mauggo ili Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema peponi.
"Hili jambo lililotokea sisi wengine tunatoa tu pole lakini mfariji mkubwa ni Mwenyezi Mungu, kwahiyo kila jambo tumtumainie na tumtegemee yeye. Kila jambo tunalolifanya tumtangulize Mungu mbele.”Amebainisha hayo Mhe. Juma.
Katika hatua nyingine Mhe. Chikoka amesema umati mkubwa umejumuika mahali hapo kutoa pole kwa wafiwa kwa sababu Marehemu alikuwa ni mtu ambae aliishi na watu kwa amani na upendo hivyo kupitia kifo chake ameacha alama ndani ya mioyo ya watu.