Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

WAHUKUMIWA BAADA YA KUKUTWA NA HATIA YA KUINGIZA MIFUGO NDANI YA PORI LA AKIBA.
10 May, 2023
WAHUKUMIWA BAADA YA KUKUTWA NA HATIA  YA KUINGIZA MIFUGO NDANI YA PORI LA AKIBA.

Mahakama ya Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro imewahukumu  Elia Lemsumba, Moono Natetwa na Juma Hassan Omary baada ya kukutwa na kosa la kuingiza mifugo yao kinyume cha sheria katika pori la Akiba Chambogo.

Kesi hiyo ya jinai Na. 80 na 84 ya mwaka 2023 imetolewa hukumu mnamo tarehe 8 Mei, 2023 katika Mahakama hiyo  baada ya watuhumiwa kukutwa na hatia.

Awali wakisoma Mashtaka, Waendesha Mashtaka wa Serikali wakiongozwa na Flavian Kalinga na  Samwel  Magoko wamesema kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa hilo mnamo tarehe 26 Aprili, 2023 mwaka huu kwa kuingiza wanyama katika pori hilo kinyume cha sheria ya misitu Na. 14 ya mwaka 2002.

Watuhumiwa hao walikuwa wakikabiliwa na makosa matano ikiwemo kuingia hifadhini, kuingiza mifugo, kuharibu uoto wa asili, kuharibu na kuvuruga biolojia ya ndani ya hifadhi na Kujenga Makazi.

Akitoa hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Same Mhe. Mussa Hamza   amemuhukumu mshtakiwa Elias Lemsumba mwenye kesi ya jinai Na. 84/2023 adhabu ya kifungo cha miaka miwili  gerezani kwa makosa yote matano.

 Mshtakiwa Moono Natetwa  mwenye kesi ya Jinai Na.84/2023 amehukumiwa kulipa faini ya kiasi cha shilingi 1,500,000/= kwa makosa yote matano pamoja na  jumla ya ng'ombe 235 kutaifishwa na kuwa mali ya Serikali.

Mshtakiwa Juma Hassan Omary mwenye kesi Na.80 ya mwaka 2023 amehukumiwa kulipa faini ya kiasi cha shilingi 1,500,000/= kwa makosa yote matano. Sambamba na hilo jumla ya ng'ombe 150 na Punda  mmoja(1) wametaifishwa kuwa mali na  Serekali ili liwe fundisho kwa wengine wenye nia ya kufanya vitendo hivyo vinavyosababisha upotevu wa rasilimali za nchi.