Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

WAENDESHA MASHTAKA WATAKIWA KUSIMAMIA SHERIA BILA KUMUONEA MTU - WAZIRI NDUMBARO
16 Apr, 2023
WAENDESHA MASHTAKA WATAKIWA KUSIMAMIA SHERIA BILA KUMUONEA MTU - WAZIRI NDUMBARO

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro  amewataka Waendesha Mashtaka na Makatibu Sheria wapya kwenda kusimamia Sheria bila kumwonea mtu wala kumpendelea mtu yeyote wakati wa utendaji wao wa kazi ili kuhakikisha haki 
inapatikana kwa usawa.

Waziri Ndumbaro amebainisha  hayo wakati akifungua Mafunzo elekezi ya awali kwa waajiriwa wapya wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka yanayofanyika mjini Morogoro kuanzia tarehe 15 hadi 21 Aprili, 2023.

Dkt. Ndumbaro amesema Waendesha Mashtaka wanapaswa kwenda kusimamia haki za msingi za kiraia kama  unyanyasaji wa kijinsia ambao ni ukatili mbaya sana na kuwataka  mtu yeyote atakayebainika kujihusisha na  vitendo hivyo kuhakikisha anahukumiwa ipasavyo.

Waziri Ndumbaro ameendelea kwa kusema Waendesha Mashtaka wanatakiwa kusimamia kwa umakini kesi zinazohusiana na mazingira na Ikolojia ambapo tabia ya watu kuingiza mifugo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa imeonekana ni mtindo wa  kawaida, kwani sheria hiyo ya mazingira imeingia kwenye makosa ya jinai.

"Tumekuwa na mgogoro mrefu Tanzania kati ya wakulima na wafugaji wakipigana na kuuana, vitendo hivyo ni jinai. Msiingie kwenye mtego wa kumpendelea mkulima wala mfugaji bali tendeni haki. Aliokiuka sheria ashughulikiwe." Ameyasema hayo Dkt. Ndumbaro.

Naye Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Joseph Pande amesema kuwa katika mwaka huu wa fedha Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imebahatika kupata jumla ya watumishi  353 ambao wote ni waajiriwa wapya wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.

"Ajira hiyo mpya ni mwendelezo wa jitihada za Serikali kuhakikisha kwamba Ofisi ya Taifa ya Mashtaka inafungua ofisi zake kila Wilaya ili wananchi waweze kupata huduma kwa ukaribu na uharaka zaidi." Amezungumza Mkurugenzi Pande.

Amesema  kazi ya Uwakili wa Serikali ni kazi nyeti  kwasababu inagusa haki za watu wengi kwa maramoja, hivyo Wakili wa Serikali asipotambua jukumu lake la kuendesha mashtaka anaweza asifikie malengo husika yaliyokusudiwa.

Aidha, Naibu Mkurugenzi amewataka waajiriwa hao wapya kujiepusha na vitendo vya rushwa kazini.

"Anayeweza kukataa rushwa ni mtu ambaye mwenye hofu ya Mungu, ukikosa kuwa na hofu ya Mungu unaingia kwenye kishawishi cha kuchukua rushwa." Ameyasema hayo Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka.