Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

USHIRIKIANO WA TAASISI TATU UMETUPA MATOKEO CHANYA - DPP
12 Aug, 2022
USHIRIKIANO WA TAASISI TATU UMETUPA MATOKEO CHANYA - DPP

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Sylvester Mwakitalu ameeleza namna jinsi ambavyo Ofisi yake ilivyoshirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai katika kupunguza kesi mbalimbali zinazotokana masuala ya jinai.

"Uhalifu hauwezi kuisha kwa taasisi moja kupambana peke yake, lakini tukishirikiana kwa pamoja tunaweza kukabiliana na uhalifu. Na kwa taarifa tulizonazo tumefanya vizuri. Ushirikiano wa hizi Ofisi tatu umetupa matokeo chanya, kwa sasa Upelelezi na uchunguzi wa makosa ya jinai unafanyika vizuri, mashtaka yanaendeshwa vizuri na matokeo tunayaona." Amezungumza hayo Mkurugenzi wa Mashtaka wakati akifanya mahojiano na Waandishi wa vyombo vya habari mara baada ya kufungua kikao cha Menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai ambacho kimefanyika leo tarehe 11 Agosti, 2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa St. Gaspar Jijini Dodoma

Pia DPP aliendelea kueleza kuwa kikao hicho ni muhimu kwa maana kinalenga kufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya kipindi cha mwaka uliopita pamoja na kuweka mikakati ya utendaji wa mwaka unaofuata na pia nikwa namna gani watashirikiana kwa pamoja kukabiliana na uhalifu.

Aidha, Mwakitalu alisema kuwa Takwimu walizonazo kwa sasa mahabusu wengi sana wamepungua kwenye magereza, na wamepungua kwasababu kesi zao zinakuwa zimefika mwisho kwa maana kuwa wamefungwa au Mahakama imewakuta hawana hatia na kuweza kuwaachia huru. Hivyo kupitia tathmini hiyo iliyofanyika na taarifa zilizopo kazi inafanyika vizuri.

Nae pia Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Kamishna wa Polisi Salum Hamduni alieleza kuwa kikao hicho ni mwendelezo wa kikao cha mwaka jana ambacho walikaa na wadau katika mnyororo wa haki jinai, hususani katika taasisi hizo ambazo zinahusika na uchunguzi na uendeshaji wa mashtaka. Na lengo la vikao hivyo ni kuhakikisha kwamba wanafanya kazi kwa pamoja katika kuhakikisha wanatoa huduma ambayo wananchi waliitarajia

"Sisi tunalenga haki za watu, kwahiyo pale ambapo tunachelewa kukamilisha upelelezi maana ake tunachelewesha haki za mtu mwingine." Amezungumza hayo Mkurugenzi Hamduni.

Pia Kamishna wa Polisi Salum aliendelea kueleza kuwa lengo kuu hasa la vikao hivyo ni kuona namna ambavyo wanaweza kuongeza tija ya ufanisi katika kuharakisha shughuli za upelelezi na uendeshaji wa mashtaka.

Hivyo basi kupitia ushirikiano huo na uratibu ambao unafanywa na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imekwenda kupunguza kwa kiwango kikubwa manung'uniko ya wananchi. Pia tathmini itakayofanyika itasaidia kuona namna ambavyo wamefanya vizuri na wapi wamekwama ili kuweza kurekebisha na hatimae kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi ambao wanawahudumia

Aidha, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kamishna wa Polisi Ramadhani Kingai ameeleza kuwa kikao hicho kina dhumuni la kuangalia ni wapi ambapo wamefikia kulingana na yale waliyoelekezana katika maazimio ya kikao kilichopita cha mwaka jana mwezi Julai. Na pia kuangalia ni wapi kuna mapungufu ili kuweza kuboresha kwa lengo la kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma bora na kupunguza malalamiko katika jamii yanayohusiana na utendaji wao wa kazi ikiwepo upelelezi kuchukua muda mrefu.

"Tumefanya kaguzi ili kubaini mapungufu haya, na sasa tupo kwenye kikao hiki ili kuweza kufanya tathmini ni kwa namna gani tunaweza kuyamaliza mapungufu haya." Amezungumza hayo Kamishna Kingai

Pia aliendelea kueleza kuwa suala la uchunguzi kuchukua muda mrefu kunatokana na sababu mbalimbali za kiutendaji, lakini kulingana na sasa muungano wao unapunguza hizo changamoto.