"Uhalifu mwingi unafanyika kwa njia ya kimtandao" Naibu DPP
Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bara Bi. Bibiana Kileo amesema uhalifu mwingi umebalidika kulingana na kasi ya Sayansi na Teknolojia inavyodizi kukuwa kwani watu wengi wanafanya uhalifu kwa njia ya kimtandao tofauti na zamani walikuwa wanafanya uhalifu kwa kutumia silaha.
Naibu DPP amebainisha hayo leo tarehe 15 Agosti, 2024 wakati akizungumza kwenye ziara ya kutembelea Ofisi ya Mkurugenzi wa Uelelezi wa Makosa ya Jinai akiwa ameambatana na Ujumbe kutoka Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar pamoja na timu nzima ya TEHAMA kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Bara kwa lengo la kujifunza na kupata uzoefu katika masuala mazima ya matumizi ya Mfumo.
Sambamba na hilo Naibu DPP Kileo ameeleza kuwa kwa sasa ulimwenguni kote asilimia kubwa wanafanya kazi ya kutekeleza majukumu yake kwa kutumia Sayansi na Teknolojia.
"Tuna nafasi nzuri ya kuendelea kujikumbusha na kuboresha mifumo yetu ya TEHAMA ili kuweza kukidhi mahitaji yote ya msingi yatakayoweza kuboresha utendaji kazi wetu hususani katika masuala ya Jinai." Amefafanua hayo Naibu DPP
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar Bi. Mwanamkaa Mohammed ameeleza kuwa Ofisi ya DPP Zanzibar wapo katika mkakati wa kuandaa na kuboresha mifumo ya TEHAMA ili kuona ni kwa namna gani watatumia vizuri teknolojia katika masuala mazima ya utendaji kazi, kwa kupitia hilo wakaona ipo haja ya yeye na timu yake kutembelea taasisi zinazojihusisha na masuala ya Haki Jinai ili kuona na kujifunza namna wanavyotumia teknolojia ili kwenda pamoja.
"Tunao mfumo lakini tunataka kuboresha zaidi pamoja na kusomana na wadau wetu kuona wamefikia wapi na kufahamu baadhi ya changamoto wanazokumbana nazo wakati wanapotumia mfumo huo kuanzia jalada linapotoka polisi, kwenda Ofisi ya Taifa ya Mashtaka hadi kufikia mahakamani." Ameyasema hayo Naibu DPP Zanzibar.
Aidha Naibu DPP Zanzibar amesema kuwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar wadau wao wakubwa ni Jeshi la Polisi kwasababu kesi nyingi zinatokea kwao.