TLS NA OTM WAKUTANA KUJADILI NAMNA BORA YA KUSHIRIKIANA KATIKA UTENDAJI KAZI.
Baraza la Uongozi wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) limefanya ziara ya kutembelea na kukutana na wajumbe wa Menejimenti wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa lengo la kujadiliana masuala mbalimbali ya kiutendaji ili kuimarisha ushirikiano na kurahisisha upatikanaji haki kwa jamii.
Katika kikao hicho Baraza hilo lenye wajumbe wapatao kumi na moja wakiongozwa na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika Wakili Boniface Mwabukusi walipata nafasi ya kuwasilisha masuala mbalimbali yenye changamoto za upatikanaji haki.
Baada ya kusikiliza hoja za Baraza la Uongozi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, wajumbe wa Menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka walitoa ufafanuzi na kueleza changamoto za kiutendaji zilizopo katika utekelezaji wa majukumu ya Mawakili binafsi ambapo walikubaliana kwa pamoja kuangalia namna bora ya kushirikiana ili kuwezesha upatikanaji wa haki.
Akizungumza katika kikao hicho Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika Wakili Bonifasi Mwabukusi aliishukuru Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa ukaribisho ambapo alitumia nafasi hiyo kutoa mapendekezo mbalimbali ya namna Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na TLS wanavyoweza kushirikiana.
Akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu alisema kikao kilichofanyika kimekuwa na manufaa makubwa na akaeleza kuwa maoni na mapendekezo yaliyotolewa kwa upande wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka yamepokelwa na yatayafanyia kazi. Pia alisihi kila mmoja kuwa makini sana wanaposhughulikia masuala ya upatikanaji wa haki kwa jamii kwa kuwa Mawakili nao ni sehemu ya jamii.
“Maoni na mapendekezo mliyowasilisha kwa upande wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka tumeyapokea na tutayafanyia kazi, yale yaliyowasilishwa lakini yanawahusu wadau wetu tutayafikisha, yale ambayo yanatekelezwa kwa ushirikiano na taasisi nyingine za haki jinai tutayafikisha na kwa pamoja kuangalia namna bora ya kuyafanyia kazi." Alisema Mkurugenzi wa Mashtaka
Akichangia maoni katika kikao hicho, Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi. Bibiana Kileo aliwataka Mawakili wanaposhughulikia masuala ya Haki Jinai au kutetea wateja wao kuzingatia ukweli na kuwa na dhamira ya dhati ya kuisaidia Mahakama kuamua kwa haki na sio kujali suala la mteja kushinda kesi pekee ili kuhakikisha kuwa haki inatendeka na mara zote kukumbuka kwamba nao ni sehemu ya jamii.
Naye Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika Bi. Laetitia Ntagazwa aliipongeza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa kazi nzuri inazozifanya katika utekelezaji wa majukumu yake.
Akitoa maoni katika kikao hicho Mkurugenzi wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika Bi. Mariam Othman aliishukuru Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa ushirikiano inaoutoa kwa kuwaruhusu Mawakili wa Serikali kushikiriki katika kazi za TLS hususani Mkutano Mkuu wa TLS na pia alitumia nafasi hiyo kuiomba Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuwawezesha Mawakili wa Serikali kushiriki katika mafunzo maalum yanayoandaliwa na TLS ili kuwajengea Mawakili weledi na kuboresha ubora wa utendaji kazi.