OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA YASAINI MAKUBALIANO (MOU) DHIDI YA KUKABILIANA NA USAFIRISHAJI HARAMU WA BINADAMU
Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imeingia Makubaliano (MOU) na Shirika lisilo la Kiserikali la Wanasheria Wasio na Mipaka (Lawyers Without Borders) juu ya utekelezaji wa Mradi wa Kukabiliana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu katika maeneo ya Upelelezi na Mashtaka.
Makubalianao hayo yamefanyika leo Jijini Mwanza kati ya Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Wanasheria Wasio na Mipaka (Lawayers Without Borders) Bi .Roben Tylor.
Akizungumza kabla ya kusaini makubaliano hayo, Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu amesema kuwa moja ya ajenda za kukabiliana nazo ni uhalifu wa kusarifisha binadamu kinyume cha Sheria ya a Haki za Binadamu.
Amesema makubaliano hayo yalipaswa kufanyika mwishoni mwa mwaka 2023 lakini kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo ilishindikana na kufanyika mwezi huu wa Januari ambapo makubaliano haya yatasaidia kuongeza na kuwajengea uelewa wapelelezi na Wachunguzi katika uendeshaji wa kesi zinazohusiana na usafirishaji wa haramu wa binadamu.
Mwakitalu amesema mahusiano ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Wanasheria Wasio na Mipaka (Laywers Without Borders) yameanza mwaka 2017 pale wanasheria kutoka taasisi ya Wanasheria Wasio na Mipaka walipotembelea ofisi ya Taifa ya Mashtaka na kuonyesha utayari wa kushirikiana kwa kutoa mafunzo kwa Waendesha Mashtaka ili kuwajengea uwezo mzuri wa kuendesha kesi zinazohusiana na usafirshaji haramu wa binadamu.
Katika hatua nyingine Mwakitalu amesema suala la Biashara ya Usafirishaji Haramu wa Binadamu limekuwa tatizo kwa nchi nyingi, kanda na duniani kote hali ambayo, nguvu ya pamoja ya kupambana na tatizo hilo inahitajika.
Ameeleza kuwa Tanzania ni moja ya nchi zinazokabiliana na tatizo hilo hivyo vita dhidi ya Usafirishaji Haramu wa Binadamu ikiwemo hatua ya kutambua na kuchukua hatua kwa wale wanaobainika kuhusika na usafirishaji huu ambapo Serikali tayari inatekeleza Sheria ya Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Binadamu ya mwaka 2008.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la Kiserikali la Wanashria Wasio na Mipaka (Lawyers Without Borders). Bi Robin Tylor amesema Makubalina hayo ina dhamira ya kuwaleta pamoja wadau wa mapambano dhidi ya biashara ya usafiriahaji haramu wa binadamu kufanya kazi kwa pamoja na kuhakikisha wahalifu na magenge ya biashara hiyo wanafikishwa mbele ya vyombo vya dola na waathirika wa biashara hizo wanapata haki.
“Juhudi hizi zitafikiwa iwapo wadau wote tutaunganisha nguvu ya kupambana dhidi ya biashara hiyo ambayo ninaamini chini ya uongozi thabiti wa Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP) na kwa kusaini makubaliano haya malengo yatafikiwa”alisema Bi. Robin
Bi. Robin ameongeza kuwa kuna haja wadau kutumia sheria ya mapambano dhidi ya Usafirishaji wa Binadamu ya Mwaka 2008 iliyofanyiwa maboresho 2022 katika kuandaa Hati za Mashtaka pale wahalifu wanapokamatwa na wakati upelelezi na ushahidi kukamilika.
Bi Robin amehitimisha hotuba yake alisema kuwa, kwa sasa dunia iko katika matumizi ya teknolojia hivyo ni vema tukajikita katika kutumia teknolojia kwenye upelelezi na ukusanyaji wa vielelezo vya kesi zinazohusiana na biashara haramu na ulinzi wa waathirika na mashahidi wa biashara hiyo.
Wakati huo huo, Robin ameishukuru Serikali ya Marekani kupitia Ofisi ya Ufuatiliaji na Upambanaji wa Biashara ya Usafirishaji Haramu wa Binadamu (J/TIP) kutoa ufadhili wa mradi huo.
Naye Mkuu wa Kikosi kasi ya Kukabiliana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu Tulibake Faidon Kasongwa amewashukuru wadau mbalimbali katika jitihada zao za kifedha na kimafunzo katika kuwajengea uwezo ndani ya Kikosi Kazi ambacho kimekuwa kikipambana na kuzuia Biashara ya Usafirishaji Haramu wa Binadamu kwa kuwa wamekuwa chachu katika utendaji kazi wao.
Kasongwa amelishukuru Shirika la Wanasheria Wasio na Mipaka (Lawyers Without Borders) kwa kuwajengea ujuzi wadau wa Haki Jinai ikiwa ni njia mojawapo ya ushirikiano na kuwawezesha kuwa na uwezo wa kuwajibika kwa haraka na kwa wakati yanapotokea masuala ya biashara haramu ya binadamu.
Amesema kuwa biashara haramu ya binadamu ni janga la dunia ambalo linahitaji ushirikiano wa wadau wote wa ndani na nje ya nchi katika kukabiliana na dhuluma zinazofanyika kupitia biashara hiyo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini Kamishna wa Polisi Salehe Ambika Mussa amesema suala la biashara haramu ya binadamu ni janga linalohitaji ushirikiano wa wadau wanaohitaji kuunganisha nguvu za pamoja ili kuweza kuyafikia mafanikio kusudiwa.
Kamishna Mussa amebainisha kuwa licha ya kuwa na jukumu kubwa la kupeleleza kesi mbalimbali kwa niaba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuhakikisha haki inatendeka, suala la biashara haramu ya binadamu ni jambo linalohitaji wadau wote kushirikiana na jeshi la polisi linapokuwa linafanya uchunguzi.
Mradi wa Kukabiliana na Biashara ya Usafirishaji Haramu wa Binadamu umeanza kutekelezwa mwezi Mei mwaka 2023 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2026. Mradi huu umelenga katika kuwajengea uwezo Waendesha Mashtaka na Watekelezaji wa Sheria katika kuendesha Upelelezi, kuratibu ushahidi,na kuendesha Mashtaka ya Makosa ya Usafirishaji Haramu wa Binadamu pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kiutendaji katika mapambano ya Usafirshaji Haramu wa Binadamu.