Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

"Mapambano dhidi ya Uhalifu tumeyapa kipaumbele" - DPP
30 Sep, 2023
"Mapambano dhidi ya Uhalifu tumeyapa kipaumbele" - DPP

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Sylvester Mwakitalu ametoa onyo kwa Watanzania ambao wanajihusisha na vitendo vya kiuhalifu na kuahidi kuongeza mikakati mipya ili kuhakikisha kwamba wanakabiliana na Uhalifu kwa nguvu zote ili wahalifu watambue kwamba uhalifu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haulipi.

Mkurugenzi Mwakitalu ameyasema hayo wakati akifungua Kikao cha Menejimenti, Wakuu wa Mashtaka, Wakuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mikoa na Wakuu wa Upelelezi Mikoa kinachofanyika tarehe 29 Septemba hadi 01 Octoba, 2023 Makao Makuu Jijini Dodoma.

Pia Mkurugenzi Mwakitalu ameeleza kuwa lengo kuu la kikao hicho ni kufanya tathmini ya utendaji kazi kwa kipindi cha mwaka mmoja kulingana na Maazimio waliyoyaweka na kuangalia ni kwa kiasi gani Maazimio hayo yametekelezeka, changamoto walizokutana nazo na sababu ya changamoto hizo, pamoja na kujadili kuweka malengo ya mwaka mwingine unaokuja.

Sambamba na hayo Mkurugenzi Mwakitalu ameeleza kuwa Makosa ya Rushwa, Uhujumu Uchumi na Ufisadi yana athari kubwa sana katika jamii kwani yanaongeza gharama za maisha na pia yanasababisha wananchi kukosa baadhi ya huduma ambazo wangeweza kuzipata. 

"Kusipokuwa na amani, kusipokuwa na utulivu hakuna mtu ambae atakwenda kufanya shughuli za maendeleo". Ameyasema hayo Mkurugenzi Mwakitalu.

Aidha, Mkurugenzi Mwakitalu ameendelea kueleza kuwa endapo Madawa ya Kulevya yataendelea kutumika pasipo kudhibitiwa basi nguvu kazi ya taifa itapotea.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Kamishna wa Polisi Salum Hamduni amesema kuwa moja ya jukumu walilonalo ni kuhakikisha wanaendelea kushirikiana na kufanya kazi kwa kwa pamoja kama timu  ili kusogeza huduma kwa wananchi hususani katika kuharakisha masuala ya uchunguzi wa uendeshaji wa mashtaka.

"Katika utekelezaji wa majukumu yetu tunagusa moja kwa moja haki za wananchi." Ameyasema hayo Mkurugenzi Mkuu Salum Hamduni.

Naye Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini  Kamishna wa Polisi Ramadhani Kingai ameeleza kuwa ushirikiano ni jambo muhimu sana katika kuwatendea haki wananchi kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.