Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

DPP AMEWATAKA WAAJIRIWA WAPYA KUFANYA KAZI KWA KUZINGATIA MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA.
01 Mar, 2024
DPP AMEWATAKA WAAJIRIWA WAPYA KUFANYA KAZI KWA KUZINGATIA MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA.

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Sylvester Mwakitalu amewataka Waajiriwa Wapya ambao ni Makatibu Sheria 36 na Mtakwimu 1 kufanya kazi kwa kuzingatia miongozo, miiko na maadili ya utumishi wa umma kwa lengo la kuisaidia Taasisi katika uendeshaji wa kazi za kiofisi.

Mkurugenzi wa Mashtaka amebainisha hayo wakati akifungua Mafunzo Elekezi kwa Waajiriwa Wapya wa Ofisi ya  Taifa ya Mashtaka (Induction Course)  yanayofanyika tarehe 26 hadi 28 Februari, 2024 Jijini Dodoma.

Pia Mkurugenzi Mwakitalu ameeleza kuwa Makatibu Sheria ndio nguzo na msingi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ambayo majukumu yake yanagusa haki za watu, hivyo maamuzi yanayofanywa na ofisi hiyo yanagusa haki za wananchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania Kampasi ya Singida Dkt. Hamisi Amani ametoa pongezi kwa uongozi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa kutenga muda na fedha kwa ajili ya kuwagharamikia watumishi wapya katika kufanya mafunzo elekezi ya awali. 

Dkt. Hamisi amesema kuwa utekelezaji wa Mafunzo Elekezi ni takwa la kisheria na kwa mujibu wa waraka wa utumishi No.5 wa mwaka 2011 umeelekeza kwamba Waajiri wote nchini wanapopata watumishi wapya wanapaswa kuwapeleka katika mafunzo elekezi ya awali.

Lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha Waajiriwa Wapya kuuelewa utumishi wa umma na misingi yake zkiwemo sera, sheria, kanuni na taratibu mbalimbali za utendaji kazi serikalini.

Sambamba na hilo Dkt. Hamisi amebainisha kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwaelimisha Waajiriwa Wapya kuyafahamu majukumu yao kwa ujumla wakiwa kama watumishi wa umma, wajibu na namna ya kuifahamu serikali jinsi inavyofanya kazi, juu ya taratibu za utendaji kazi serikalini, maadili, nidhamu, uadilifu na ustahimilifu.

"Kwa kada ya Makatibu Sheria wanayo nafasi kubwa ya kutekeleza jukumu la serikali la kuhudumia wananchi kwasababu mnapotekeleza majukumu yenu mnakutana moja kwa moja na wananchi hivyo mna kila sababu ya kuzingatia nidhamu, uadilifu na kuwa wastahimilifu kwasababu ya vishawishi mbalimbali vinavyoweza kutokea." Amefafanua hayo Dkt. Amani.

Aidha Mkurugenzi Amani ameeleza kuwa Serikalini imeyapa umuhimu mkubwa sana mafunzo hayo elekezi ya awali kwasababu watumishi ambao wanaingia moja kwa moja na wakaendelea kufanya kazi kwa muda mrefu bila kupatiwa mafunzo hayo inatarajiwa hawataweza kutekeleza majukumu kwa ufanisi zaidi na kuwa na utendaji kazi hafifu, uvunjaji wa taratibu za utendaji kazi na migogoro katika utendaji kazi.