Habari

Imewekwa: May, 31 2022

NAIBU WAZIRI WA KATIKA NA SHERIA AZINDUA MWONGOZO WA KIUTENDAJI WA UPELELEZI NA UENDESHAJI WA KESI ZA RUSHWA

News Images

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Geophrey Mizengo Pinda amezindua Mwongozo wa Kiutendaji wa Upelelezi na Uendeshaji wa Kesi za Rushwa ambao umetolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka chini ya kifungu cha 18 na 24 vya Sheria ya Usimamizi wa Mashtaka, Sura ya 430 nchini.

Uzinduzi huo ameufanya kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro leo Mei 31, 2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Mheshimiwa Geophrey Pinda ameeleza kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria itashirikiana kwa karibu na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika kuhakikisha mfumo bora wa utoaji haki kwa wananchi unazidi kuimarika na kuleta ufanisi.

"Mahakama ya Tanzania imefanya mabadiliko makubwa sana, lakini haiwezi kuperfom kama nyie hamna vitendea kazi vya kusaidia kesi zao kwenda, kwa hiyo tumekubalina kwenye Mpango wa Serikali tunakuja na mageuzi makubwa na ya idara zote zinazosaidia katika huduma za utoaji haki." Ameyasema hayo Mizengo Pinda

Pia ameongeza kuwa, dhamira ya Serikali ni kuendelea kuwa na mfumo mzuri wa utoaji haki kwa wananchi hivyo ushirikiano wa dhati wa Wizara hizo ni muhimu sana ili kuwawezesha wananchi kupata haki zao pamoja na kuendesha shughuli za maendeleo kwa ufanisi.

Nae pia Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Sylivester Mwakitalu amewapongeza wadau wa maendelo ikiwemo Serikali ya Uingereza na Umoja wa Ulaya ambao wameshiriki kikamilifu kufanikisha juhudi mbalimbali za Serikali katika kupambana na vitendo vya rushwa.

DPP alieleza kuwa, upelelezi wa makosa ya rushwa unahitaji umakini wa hali ya juu kutokana na makosa hayo kufanywa na watu wenye weledi, hivyo upelelezi wake unahitaji umakini na umahiri ndiyo maana Ofisi ya Taifa ya Mashitaka kwa kushirikiana na wadau waliona ni vyema wakatengeneza mwongozo huo ambao utawasaidia Wapelelezi na Waendesha Mashtaka wanapoendesha kesi hizo ili kuleta usawa.

"Kwa kipindi ambacho tuliwapatia madaraka Waendesha Mashtaka wa Mikoa na Wilaya tuligundua ziko changamoto za hapa na pale hati za Mashtaka za mahali pamoja zinatofautiana na hati za Mashtaka za sehemu nyingine, na namna uchunguzi unavyopita sehemu moja na sehemu nyingine kwa hiyo tukaona kwa kushirikiana pamoja tutengeneze mwongozo ambao utawaongoza waendesha Mashtaka na Wapelelezi ili waweze kufanya kazi hiyo kwa weledi, lakini tupate tija na pia tupate matokeo chanya." Ameyasema hayo DPP Mwakitalu

Mkurugenzi Mwakitalu alieleza kuwa Mwongozo uliozinduliwa hautosaidia kubadilisha dira, bali taratibu zilizopo ni nyongeza ya kile ambacho tayari kipo na kitasaidia Watumishi wote ambao watashiriki katika mapambano dhidi ya rushwa.

DPP aliendelea kueleza kuwa mwongozo utawawezesha Wapelelezi na Waendesha Mashtaka kushughulikia kesi za rushwa kwa urahisi na tija, na mara baada ya kuzinduliwa utasambazwa na kuhakikisha kwamba watendaji wote wanaupata na pale itakapolazimika kufanya mafunzo ili kurahisisha wauelewe na wautumie kikamilifu basi itafanyika hivyo.

"Mwongozo huu ni nyenzo muhimu sana kwetu kwani utatusaidia kupata matokeo chanya katika kupambana na rushwa." Ameyasema hayo DPP Mwakitalu.

Aidha, Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Joseph Pande amesema kuwa, mwongozo huo utasaidia kwa kiwango kikubwa ikiwemo kuongeza mahusiano kuanzia tukio linapotokea mpaka kesi itakapomalizika mahakamani.

Nae pia Mkurugenzi wa Divisheni ya Makosa ya Udanganyifu, Utakatishaji Fedha na Rushwa kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Bw. Oswald Tibabyekomya ameeleza kuwa, Mwongozo wa Kiutendaji wa Upelelezi na Uendeshaji wa Kesi za Rushwa (Standard Operating Procedures for Investigation and Prosecution of Corruption and Related Offences), umetolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka chini ya kifungu cha 18 na 24 vya Sheria ya Usimamizi wa Mashtaka, Sura ya 430 (The National Prosecutions Service Act, Cap 430).

Vifungu ambavyo amesema, vinampa Mkurugenzi wa Mashtaka mamlaka ya kutengeneza miongozo kwa ajili ya kuratibu upelelezi na kusimamia mashtaka.

"Lengo la Mwongozo huu ni kuweka mfumo unaofanana wa kupeleleza na kuendesha mashtaka kwa kuelekeza masuala muhimu ya kuzingatia na kutengeneza nyenzo kama vile mpango wa uchunguzi (Investigation Plan), Uendeshaji Mashtaka ( Prosecution Plan) na Uchambuzi wa Viini vya Makosa ya Rushwa (Elements Worksheet) ambavyo vitasaidia kuweka utaratibu unaofanana katika kushughulikia kesi hizi." Amefafanua hayo Mkurugenzi Oswald

Pia Mkurugenzi Tibabyekomya aliendelea kueleza kuwa, mambo muhimu yanayosisitizwa katika mwongozo ni Kushauriana na Kuratibu Kesi Kubwa za Rushwa Mapema ( Early Case Consultation and Coordination).

"Katika eneo hili Mwongozo unawataka Wachunguzi baada ya kujiridhisha kuwa kosa limetendeka, kutoa taarifa kwa Viongozi wa Mashtaka kwenye Ofisi za Taifa za Mashtaka ngazi ya Wilaya na Mikoa au kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ili waweze kuteua Mwendesha Mashtaka kuratibu upelelezi huo.

Na Mwendesha Mashtaka atakayeteuliwa atashirikiana na wachunguzi kwenye hatua zote muhimu za upelelezi kwa ajili ya kuhakikisha ushahidi wenye ubora unakusanywa ili kuwezesha kuwa na matokeo mazuri mahakamani." Amezungumza hayo Bw. Oswald.

Pia ameeleza kuwa ili kuhakikisha kunakuwepo na uratibu mzuri, mwongozo unataka wachunguzi na Waendesha Mashtaka kufanya vikao vya pamoja kabla na baada ya kukamata watuhumiwa (pre-arrest conference, post arrest conference) au wakati wowote linapotokea jambo la dharura (emergency conference) kwa ajili ya kujadili mwenendo na masuala muhimu ya upelelezi.

Katika, mwongozo huo, Mkurugenzi Tibabyekomya anasema, wakati wa ukusanyaji ushahidi mwongozo unafafanua utaratibu wa kufuata wakati wa ukamataji, upekuzi na ukusanyaji wa ushahidi wa aina mbalimbali kama vile uchukuaji wa maelezo ya mashahidi, maelezo ya washtakiwa ushahidi wa kitaalam ili kuhakuikisha ushahidi unakusanywa kwa kuzingatia sheria.

Upelelezi wa Mburulo wa Kifedha ( Financial Investigation).

Kwa kuzingatia kuwa, makosa ya rushwa ni makosa ambayo yanatendeka kwa ajili ya kupata fedha au mali, amesema mwongozo unawataka wachunguzi kufanya uchunguzi wa mali mapema wanapoanza uchunguzi wa makosa ya rushwa ili waweze kubaini mali hizo na kuchukua hatua stahilifu mapema

Ili kuhakikisha maamuzi yanatolewa baada ya kuelewa vizuri ushahidi, Mwongozo unasisitiza kufanya vikao vya majadiliano kati ya Wachunguzi na Waendesha Mashtaka wakati jalada linapowasilishwa Ofisi za Taifa za Mashtaka au baada ya kuwa jalada limepitiwa na waendesha mashtaka katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka. Vikao hivi vinaweza kuombwa na Wachunguzi au kuitishwa na Waendesha Mashtaka wanapoona kuna jambo linalohitaji majadiliano

Baada ya upelelezi kukamilika na kesi kufunguliwa mahakamani Mwongozo unawataka wachunguzi na waendesha mashtaka kufanya maandalizi vizuri kabla ya kesi kuanza kusikilizwa kwa kufanya vikao kabla ya kesi kuanza (pre-trial conference) kati ya wachunguzi na waendesha mashtaka. Mwongozo pia umetengeza nyenzo (templates) kama vile nyenzo za kutumia kuwatayarisha na kuwaongaza mashahidi mahakamani na nyenzo ya kutumia kutoa vilelezo mahakamani kwa ajili ya kuahakikisha maandalizi mazuri yanafanyika.

Mwongozo pia umetengeneza nyaraka ya uchambuzi wa makosa yote yaliyopo katika Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ambayo inachambua viini vya makosa hayo na kutoa mifano ya hati za mashtaka. Lengo la kutengeneza nyenzo hii ni kuhakikisha wachunguzi na waendesha mashtaka wanaelewa vizuri viini vya makosa ili viwasaidie wakati wa upelelezi, maandalizi ya hati za mashtaka na wakati wa uendeshaji wa kesi mahakamani.

Kwa upande wao wawakilishi wa mabalozi, Bw.Simon Charter kwa niaba ya Balozi wa Uingereza nchini Tanzania na Simon Van Broek kwa niaba ya Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania wamesema kuwa, wataendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania katika kupambana na vitendo vya rushwa.

Sambamba na shughuli mbalimbali za maendeleo Ili iweze kutekeleza kikamilifu miradi mbalimbali ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.