Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

NAIBU KATIBU MKUU AZINDUA TAARIFA YA UKAGUZI WA VIZUIZI WANAKOSHIKILIWA WATOTO WALIOKINZANA NA SHERIA
27 Jul, 2022
NAIBU KATIBU MKUU AZINDUA TAARIFA YA UKAGUZI WA VIZUIZI WANAKOSHIKILIWA WATOTO WALIOKINZANA NA SHERIA

Naibu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Khatibu Kazungu amefanya uzinduzi wa Taarifa ya Ukaguzi wa Vizuizi wanakoshikiliwa Watoto waliokinzana na Sheria ambao umefanyika tarehe 18 Julai, 2022 Jijini Dodoma.

Katika hafla ya uzinduzi huo Dkt. Khatibu ameeleza kuwa mtoto ndio taifa la leo hivyo wasipowekeza kwenye maeneo ya watoto katika kiafya, kielimu na kiakili zaidi basi taifa hili litaangamia zaidi.

"Uwekezaji katika maeneo haya ni muhimu sana kwa watoto wetu, na ni moja ya sababu ambazo zinapelekea watoto hawa 435 kukutwa katika maeneo mbalimbali ya vizuizi hapa Tanzania. Hivyo juhudi zozote zinazolenga kuhusu ustawi wa watoto hazina budi kupongezwa." Amezungumza hayo Dkt. Kazungu

Aidha Naibu Katibu Mkuu alitoa pongezi kwa niaba ya Wizara ya Katiba na Sheria kuipongeza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa kuona umuhimu wa kukagua vizuizi hivyo kwa lengo la kulinda watoto walio kwenye mkinzano wa vyombo vya sheria. Pia alitoa pongezi kwa wadau wote walioshirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka katika kukamilisha zoezi hilo kwa mafanikio makubwa

Pia Dkt. Kazungu aliendelea kueleza kuwa matokeo yaliyofanyika ya ukaguzi huo ni vema yatumike kama kizio cha kaguzi zitakazoendelea ili kuweza kuona kama wanasonga mbele ama hawajaweza kuimarisha haki za watoto.

"Natambua jukumu la haki jinai sio la Wizara ya Katiba na Sheria peke yake, hivyo ni imani yangu kuwa wadau wote mlio katika mnyororo huu tutashirikiana kikamilifu katika utekelezaji wa yale yote yaliyomo ndani ya taarifa hii ambayo tunakwenda kuizindua leo hii na katika taarifa zitakazokuwa zinakuja kadri tutakavyosonga mbele." Ameyasema hayo Naibu Katibu Mkuu

Nae pia Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu alieleza kuwa katika ukaguzi wao walioufanya kwa kipindi hicho walikuta watoto 435 wakitunzwa kwenye Taasisi mbalimbali ambazo zimepewa majukumu kisheria. Na kati yao watoto 46 walikuwa hawajakinzana na sheria ambao wapo mahabusu kwasababu ya wazazi wao wameshikwa kwa makosa mbalimbali ambao pia ni watoto wadogo wasioweza kutenganishwa na wazazi wao. Pia walikuta watoto 260 wapo kwenye Magereza ambapo kati yao tayari wapo hatiani kutumikia vifungo vyao na wengine kesi zao zilikuwa zikiendelea kwahiyo wapo mahabusu. Na kwa upande wa kwenye shule ya marekebisho watoto waliokuwepo ni 40, kati yao watoto 38 walikuwa ni watoto wa kiume na watoto 2 ni mabinti.

Aidha, Mkurugenzi Mwakitalu aliendelea kueleza kuwa katika ukaguzi huo hawakuishia kuona watoto walioko kwenye Taasisi hizo bali walisonga mbele zaidi ili kuweza kufahamu sababu zinazowafanya watoto hawa kuingia kwenye ukinzani na sheria na wakaweza kubaini kuwa chanzo kikubwa ni yalikuwa ni malezi.

"Watoto wengi ambao wameingia katika changamoto hii tumebaini wanatoka katika familia ambazo zina migogoro. Na pia tumebaini kuwa watoto wengi wanaoingia kwenye shida hii ni wale ambao hawapo shule au wanaenda shule kwa kusuasua. Hii yote ni sababu ya kukosa malezi mazuri kutoka kwa wazazi na jamii." Ameyasema hayo DPP.

Pia DPP aliendelea kueleza kuwa wapo watoto ambao kwasababu mbalimbali hawapo pamoja na wazazi wao. Na jamii ina jukumu la kuhakikisha watoto hawa wanapata malezi na kupata haki

zao zote za msingi.

Aidha, Kaimu Mkurugenzi Divisheni ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Bw. Tumaini Kweka alieleza kuwa Taarifa hiyo inahusu ukaguzi wa vituo na maeneo ambayo wanashikiliwa watoto waliokinzana na sheria, ambayo inahusu magereza, Mahabusu za Polisi na inahusu shule maalum za mafunzo ya watoto pamoja na nyumba maalum ambapo watoto hao waliokinzana na sheria wanashikiliwa.

Pia Mkurugenzi Kweka aliendelea kusema kuwa Taarifa hiyo inahusisha zoezi ambalo lilifanyika mwishoni mwa mwaka 2021 pamoja na mwanzoni mwa mwaka 2022 ambapo timu maalum kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ilikwenda kutembelea maeneo hayo chini ya ufadhili wa UNICEF ili kuangalia ni kwa namna gani sheria ya mtoto ya mwaka 2009 inatekelezwa dhidi ya watoto hao ambao wamekinzana na sheria.

Na baada ya ukaguzi huo timu iliweza kuandaa Taarifa ikiainisha maeneo mbalimbali kuhusiana na utekelezaji wa sheria ya mtoto pamoja na matamko mbalimbali ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa. Na ni kwa namna gani yalikuwa yanatekelezwa katika kuhakikisha haki na ustawi wa mtoto ambae amekinzana na sheria.