Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

MIAKA 20 JELA KWA KOSA LA KUPATIKANA NA NYARA ZA SERIKALI
02 Jul, 2026
MIAKA 20 JELA KWA KOSA LA KUPATIKANA NA NYARA ZA SERIKALI

Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro, Mkoa wa Manyara, imemhukumu Regani Longidare kutumikia kifungo cha miaka 20 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na nyara za Serikali, ambazo ni nyama za twiga wawili zenye thamani ya shilingi 97,320,000.

Hukumu hiyo imesomwa leo, tarehe 30 Juni 2026, na Hakimu Mkuu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Charles Uiso, baada ya Mahakama kuridhika kuwa upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi wa kutosha kuthibitisha shtaka hilo pasipo kuacha shaka yoyote.

Katika Shauri la Uhujumu Uchumi Na. 472 la mwaka 2026, ilielezwa kuwa mnamo tarehe 16 Desemba 2025, katika eneo la Sukuro lililopo ndani ya Pori Tengefu la Simanjiro, Wilaya ya Simanjiro, Mkoa wa Manyara, mshtakiwa alipatikana akiwa na nyama za twiga wawili pamoja na vichwa na ngozi zinazolingana na twiga hao waliouawa, ambao ni mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mtuhumiwa alitenda kosa hilo kinyume na matakwa ya Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori kwa kuwa hakuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Katika kuithibitisha kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi saba na vielelezo saba vilivyoiwezesha Mahakama kufikia uamuzi wa kumtia hatiani mshtakiwa.

Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, Mahakama ilibaini kuwa upande wa mashtaka umethibitisha shtaka hilo pasipo kuacha shaka yoyote. Mbali na kumhukumu kifungo cha miaka 20 gerezani, Mahakama pia iliamuru pikipiki iliyokuwa ikitumiwa na mshtakiwa wakati wa kutenda kosa hilo itaifishwe na kuwa mali ya Serikali.

Kesi hii iliendeshwa na Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.