Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

ALIYEKUWA MENEJA WA TRA AFUNGWA MIAKA 20 JELA
02 Jul, 2026
ALIYEKUWA MENEJA WA  TRA AFUNGWA MIAKA 20 JELA

Mahakama  ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kigoma imemhukumu aliyekuwa Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Wilaya ya Kibondo, bwana Irving Bagasheki (40) kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la kukutwa na Nyara za serikali ambazo ni meno mawili ya tembo yenye thamani ya shilingi milioni 52 na kosa la pili kujihusisha isivyo Halali na Nyara za Serikali.

Hukumu hiyo imesomwa tarehe 29 Juni, 2026 na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mhe. Aristida Tarimo baada ya kuridhika na ushahidi uliowasilishwa na upande wa Mashtaka.

Katika kesi hiyo ya Uhujumu Uchumi Na. 4733 ya mwaka 2024 Mshtakiwa ambaye alikuwa Meneja wa TRA Wilaya ya Kibondo alikuwa anakabiliwa na mashtaka mawili ambapo shtaka la kwanza ni kukutwa na Nyara za Serikali na shtaka la pili ni kujihusisha na Nyara isivyo Halali kinyume Sheria ya  Uhifadhi wa Wanyama Pori.

Imeelezwa mahakamani hapo kuwa mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo  mnamo tarehe 1 Julai, 2024 huko katika kizuizi Cha Kihomoka kilichopo Wilaya ya Kakonko ndani ya Mkoa wa Kigoma ambapo alikamatwa akijaribu kusafirisha meno hayo mawili ya tembo na kufikishwa kituo cha polisi Wilaya ya Kakonko

Upande wa mashtaka uliwasilisha jumla ya mashahidi 17 pamoja na vielelezo 23.

Baada ya kusikiliza ushahidi kutoka pande zote mbili, Mahakama imeridhika kuwa upande wa Jamhuri umethibitisha kosa dhidi ya mshtakiwa  bila kuacha shaka hivyo kumkuta mshtakiwa  na hatia na kumpa adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela kwa Kila Kosa ambapo Adhabu hiyo utakwenda kwa Pamoja.

Kesi hii imeendeshwa na Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.