WIZARA, NPS KUIMARISHA MSHIKAMANO KWA MASLAHI YA WANANCHI
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Seif Shekalaghe, amesisitiza juu ya kuimarisha ushirikiano kati ya Wizara hiyo na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), katika masuala mbalimbali ya kiutendaji kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati.
Akizungumza wakati alipotembelea Ofisi hiyo tarehe 13 Agosti, 2026, Makao Makuu ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kutembelea taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo Dkt. Seif amesema NPS ni taasisi muhimu katika mnyororo wa haki jinai, kutokana na nafasi yake ya kupokea na kuchakata majalada ya uchunguzi, kuendesha mashauri mahakamani na kuhakikisha haki inapatikana kwa wananchi kwa wakati na kwa usawa.
Aidha, Dkt. Shekalaghe ametambua na kupongeza mchango wa watumishi wote wa NPS katika kutekeleza majukumu yao, akisisitiza kuwa mafanikio ya Ofisi hiyo hayawezi kutegemea juhudi za Mkurugenzi wa Mashtaka pekee, bali yanatokana na ushirikiano na weledi wa watumishi wote.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo amewahimiza watumishi kuendelea kuzingatia Dira ya Ofisi hiyo inayosisitiza utoaji wa huduma za mashtaka kwa wakati na usawa kwa wote, akieleza kuwa utekelezaji wa misingi hiyo ni muhimu katika kuhakikisha kila mwananchi anapata haki bila kujali hali yake ya maisha au nafasi yake katika jamii.
Amesema utekelezaji wa Dira hiyo unaendana na juhudi za Serikali za kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati na huduma za kisheria zinawafikia wananchi kwa ukaribu zaidi, ikiwemo kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC), inayolenga kuwafikia wananchi wenye uhitaji wa huduma za kisheria bila malipo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mashtaka, Bw. Sylvester Mwakitalu, ameishukuru Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuiwezesha NPS kupiga hatua katika utekelezaji wa majukumu yake, ikiwemo upanuzi wa huduma za kimashtaka nchini.
Amesema kwa sasa NPS imefanikiwa kufungua ofisi katika makao makuu ya mikoa yote Tanzania Bara, Ofisi nne (4) za Mikoa ya Kimashtaka na wilaya 93, huku ikiendelea na mpango wa kufungua ofisi katika wilaya zote nchini. Aidha, NPS inaendelea kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma kwa kujenga na kukarabati majengo ya ofisi za mikoa na wilaya, ambapo baadhi ya miradi imekamilika na mingine inaendelea.
Mwakitalu amesema jukumu kubwa la NPS ni kusimamia mashtaka ya jinai katika mahakama zote nchini, kuanzia Mahakama ya Mwanzo hadi Mahakama Kuu, pamoja na kuratibu shughuli za upelelezi zinazofanywa na taasisi mbalimbali za Serikali.
