Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA

MWONGOZO WA CHAPA (BRANDING MANUAL) WA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA WAZINDULIWA RASMI
24 Oct, 2025
MWONGOZO WA CHAPA (BRANDING MANUAL) WA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA WAZINDULIWA RASMI

Mkurugenzi wa Mashtaka, Bw. Sylvester Mwakitalu, amezindua rasmi Mwongozo wa Chapa (Branding Manual) wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), unaolenga kutoa matumizi sahihi ya chapa ya ofisi katika nyanja zote za mawasiliano ya ndani na nje ya Ofisi.

Uzinduzi huo umefanyika leo Oktoba 23, 2025 katika kikao cha Menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kinachoendelea, mkoani Morogoro.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, DPP Mwakitalu ameeleza kuwa mwongozo huo ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha utambulisho wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka unakuwa wa kitaalamu, thabiti, na unaoendana katika shughuli mbalimbali za kiofisi.

“Mwongozo huu utaimarisha utambulisho wetu wa taasisi na kuhakikisha mawasiliano yetu yanakuwa na ufanano, heshima, na ubora unaoakisi majukumu yetu ya kisheria na kitaifa,” alisema DPP, Mwakitalu.

Mwakitalu, amewataka watumishi wote wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kote nchini kuzingatia na kuufuata mwongozo huo kikamilifu katika matumizi ya nembo, nyaraka rasmi, mavazi ya kikazi, matangazo, machapisho, na majukwaa ya kidijitali.

“Ni wajibu wa kila mtumishi kuhakikisha chapa ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka inalindwa na kutumika ipasavyo’’, Alisisitiza DPP, Mwakitalu.