JUKWAA LA HAKI JINAI TAIFA LAFANYA TATHMINI YA UTENDAJI KAZI
Jukwaa la Haki Jinai Taifa limekutana kufanya tathmini ya utendaji kazi kwa lengo la kusikiliza changamoto zinazojitokeza katika mnyororo wa haki jinai na kwa pamoja kutafuta suluhu zitakazoboresha utoaji wa haki kwa wananchi, hususani katika usimamizi wa mashtaka na mifumo inayohusiana na haki jinai kwa ujumla.
Mkutano huo umefanyika tarehe 30 Januari, 2026, katika Ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) Makao makuu, jijini Dodoma, ukihusisha viongozi na wawakilishi wa taasisi zinazounda Jukwaa la Haki Jinai Taifa, kwa lengo la kujadili kwa kina masuala ya kiutendaji yanayoathiri utoaji wa haki katika ngazi za kitaifa, mikoa na wilaya.
Akizungumza wakati wa kufungua mkutano huo, Sylvester Mwakitalu, Mkurugenzi wa Mashtaka, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Haki Jinai Taifa, alisema mkutano huo umejikita katika kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo uchakavu wa miundombinu katika baadhi ya magereza, uhaba wa shule za maadilisho, pamoja na upungufu wa vifaa vya TEHAMA katika taasisi zinazounda Jukwaa hilo.
“Mkutano huu umetupa nafasi ya kujadili masuala yanayogusa moja kwa moja taasisi zetu, mnyororo mzima wa haki jinai na shughuli ambazo kwa pamoja tunaazimia kuzitekeleza ili kuboresha huduma kwa wananchi,” alisema Mwenyekiti Mwakitalu, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano na uwazi miongoni mwa wadau wa haki jinai.
Katika mkutano huo, wajumbe waliwasilisha taarifa za utekelezaji wa majukumu katika taasisi zao ngazi za mikoa na wilaya, kwa lengo la kuzitathmini, kupata uzoefu wa pamoja na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.
Aidha, Jukwaa la Haki Jinai Taifa liliazimia maswala mbalimbali ikiwemo; kuchukua hatua za pamoja kutatua changamoto za kimtandao kwa wadau wote wa haki jinai ili kuimarisha uendeshaji wa mashauri kwa njia ya mtandao (video conference), kuendelea kuboresha miundombinu ya magereza nchini, kuongeza wataalamu wenye taaluma za kisayansi ili kuharakisha upelelezi na chunguzi, pamoja na kufanya utaratibu wa kupata suluhisho la kudumu kuhusu mahabusi na wafungwa kupata matibabu bila malipo na kuimarisha ulinzi mipakani ili kudhibiti uingizwaji wa madawa ya kulevya nchini.
Vilevile Jukwaa la Haki Jinai Taifa ni jukwaa la ushirikiano linalojumuisha taasisi za mnyororo wa haki jinai ikiwemo; Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), Jeshi la Polisi, Mahakama, Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Magereza, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Idara ya Ustawi wa Jamii, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Bodi ya Parole, Idara ya Huduma kwa Jamii, Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Katiba na Sheria, kwa lengo la kuratibu na kuimarisha utekelezaji wa haki jinai kwa maslahi ya wananchi.
