Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

CHANGAMOTO ZISIWE KIKWAZO CHA KUACHA KUUTUMIA MFUMO - KAIMU NAIBU DPP
26 Feb, 2022
CHANGAMOTO ZISIWE KIKWAZO CHA KUACHA KUUTUMIA MFUMO - KAIMU NAIBU DPP

Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka ambae pia ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Usimamizi wa Kesi na Uratibu wa Upelelezi Bi. Neema Mwanda amewataka Wakuu wa Mashtaka wa Wilaya na Waendesha Mashtaka Viongozi kutokuacha kuutumia mfumo wa kielekitroniki sababu ya changamoto yoyote ile itakayotokea wakati wakitumia mfumo huo kwani changamoto ni sehemu ya kuendelea kujifunza na hutokea katika mfumo wowote ule. Na endapo watakutana na changamoto yoyote ile basi wasisite kutoa taarifa kwa viongozi husika wa mfumo huo.

"Tutakapoanza kuutumia mfumo huwa kuna changamoto nyingi ambazo pia ni sehemu ya kujifunza, changamoto hizi zisiwe kikwazo cha kuacha kuutumia mfumo wetu."

Amezungumza hayo Kaimu Mkurugenzi Mwanda wakati akihitimisha Mafunzo ya Utumiaji wa Mfumo wa Kielektroniki wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka katika masuala ya kesi kwa Wakuu wa Mashtaka wa Mikoa na Wilaya pamoja na Waendesha Mashtaka Viongozi yaliyoanza tarehe 22 Februari, 2022 na kumalizika tarehe 25 Februari, 2022 Jijini Dar es Salaam katika ofisi za TAGLA zilizopo Chuo Kikuu cha Usimamizi wa Fedha (IFM)

Aidha, Kaimu Mkurugenzi alieleza kuwa kuanzishwa kwa mfumo huu kumelenga kupunguza gharama za uzalishaji, kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma pasipo kujali muda wala sehemu ya kijografia, ikiwa ni pamoja na kuongeza uwazi na kupunguza mianya ya rushwa kwenye taasisi.

Pia Kaimu Mkurugenzi alitoa wito kwa washiriki wa mafunzo hayo kuwa anawasihi na kuwaomba kwenda kuufanyia kazi mfumo huo vizuri na kutoa elimu kwa wengine waliopo katika vituo vyao vya kazi.