Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

NAIBU MKURUGENZI WA MASHTAKA AMEWATAKA WATUMISHI WA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA KUFANYA KAZI KWA KUZINGATIA HAKI
08 May, 2024
NAIBU MKURUGENZI WA MASHTAKA AMEWATAKA WATUMISHI WA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA KUFANYA KAZI KWA KUZINGATIA HAKI

Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi. Bibiana Kileo amewataka watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kufanya kazi kwa kuzingatia haki, ushirikiano kwa lengo la kusukuma gurudumu la maendeleo ya Jamii na Taifa kwa ujumla.

Naibu Mkurugenzi amebainisha hayo mapema tarehe 30 Aprili, 2024 wakati akizungumza na Menejimenti na Watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu Jijini Dodoma alipowasili kwa mara ya kwanza tangu kuapishwa kwake.

"Namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini na kuniteua kuwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka,  ninaahidi kujitahidi kwa uwezo wangu wote kusaidia majukumu yako kwa weledi na uadilifu mkubwa." Amesema Mkurugenzi Bibiana.

Naibu Mkurugenzi amesema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ina jukumu la kikatiba chini ya Ibara 59B ya kusimamia Uendeshaji wa Mashtaka nchini na jukumu hili linapaswa kufanyika kwa kuzingatia misingi ya haki na maslahi makubwa ya umma. Ofisi hiyo pia imepewa jukumu kubwa la kuamua juu ya hatma za watu, maisha ya watu hivyo watumishi hao wanapaswa kufanya kazi kwa weledi mkubwa, kuzingatia sheria bila kuwa na upendeleo wala kumwonea mtu.

"Niwaombe tushirikiane pamoja katika kutimiza jukumu hili ili kuifanya taasisi yetu kuwa bora na inayoongoza kwa kutenda haki ndani ya nchi hii." Amefafanua hayo Naibu Mkurugenzi.

Sambamba na hilo Naibu Mkurugenzi ametoa pongezi kwa Uongozi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa ushirikiano wanaoutoa kwa kupambana usiku na mchana ili kuifanya taasisi izidi kusonga mbele ili kuwawezesha wananchi kupokea huduma wanazostahili kutoka kwao ambapo imepelea kupunguza malalamiko kwa wananchi na kesi kusikilizwa kwa wakati.