Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

WAWILI WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUMDANGANYA DPP KUWA NI MAOFISA USALAMA WA TAIFA
19 Jun, 2021
WAWILI WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUMDANGANYA  DPP KUWA NI  MAOFISA USALAMA WA TAIFA

Mfanyabiashara, Joshua Jelemia (37) na Yahaya Abdallah (31) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es salaam kujibu mashtaka mawili ya kujifanya Maofisa Usalama wa Taifa (TISS) katika ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) na naibu mkurugenzi wa mashtaka.

Washtakiwa hao wamefikishwa katika Mahakama hiyo Juni 18, 2021 na kusomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Godfrey Isaya.

Wakiwasomewa Mashtaka na wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amedai kuwa watuhumiwa hao walitenda makosa hayo Juni 12, 2021 katika ofisi za DPP zilizopo jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Inadaiwa siku hiyo wawili hao walifika Ofisini kwa (DPP) Slyvester Mwakitalu na naibu wake (DDPP), Joseph Pande na kujitambulisha kuwa wao ni maofisa kutoka TISS.

Baada ya kusomewa Mashitaka hayo, upande wa Mashtaka umedai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na hivyo wapangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea washtakiwa hoja za awali. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 22, 2021 na washtakiwa kurudishwa rumande baada ya kukosa dhamana.