Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

NAIBU KATIBU MKUU NA DPP WATEMBELEA MAGEREZA YA MKOA WA LINDI KESI 16 ZAFUTWA NA DPP
28 Aug, 2019
NAIBU KATIBU MKUU NA DPP WATEMBELEA MAGEREZA YA MKOA WA LINDI KESI 16 ZAFUTWA NA DPP

NAIBU KATIBU MKUU NA DPP WATEMBELEA MAGEREZA YA MKOA WA LINDI KESI 16 ZAFUTWA NA DPP

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Amon Mpanju na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) Bw. Biswalo Mganga wametembelea magereza ya wilaya za Lindi, Nachingwea na Ruangwa mkoani Lindi na kufuta kesi 16 zilizokuwa zikiwakabili mahabusu mbalimbali waliokuwa ndani ya magereza hayo .

Kesi hizo zilizofutwa zinajumuisha kesi ndogondogo ambazo zinaweza kumalizwa nje ya Mahakama kama vile kutukana, wizi wa vitu vidogo vidogo na kupigana, kesi zilizokosa ushahidi na kusababisha watuhumiwa kukaa gerezani kwa muda mrefu zikiwemo za mauaji.

Bw. Mpanju na DPP wametembelea magereza hayo na kuzungumza na wafungwa na mahabusu walioko katika magereza hayo na kujionea hali halisi ilivyo ndani ya magereza hayo na kutumia mamlaka yake kisheria kufuta baadhi ya kesi ambazo amejiridhisha kukidhi matakwaya kuzifuta na hivyo kusaidiakupunguza msongamano wa mahabusu katika magereza hayo.

Bw. Mpanju amesema kazi ya kutembelea magereza kukagua na kuzungumza na wafungwa na mahabusu ni miongoni mwa majukumu ya kisheria ya Wizara na Ofisi ya DPP kwani huziwezesha ofisi hizo kutambua matatizo ya kisheria yanayowakabili wafungwa na mahabusu na hivyo kuwasaidia kwa kuwapa msaada wa kisheria na kuwawezesha kupata haki zao wanazostahili.

Bw. Mpanju amewataka mahabusu waliofutiwa kesi zao kubadili mienendo yao na kuwa raia wema na washiriki kikamilifu katika kazi za ujenzi wa taifa.

Wafungwa na mahabusu katika magereza hayo wamelalamikia kuchelewa kupata haki zao kulazimika kutoa maelezo mbele ya polisi bila ya kuwepo ndugu zao au mlinzi wa amani, kuchelewa kupata hati za nakala za hukumu, upelelezi wa kesi zao kuchelewa na hivyo kuchukua muda mrefu, kukosa nafasi ya kupewa adhabu mbadala kama viboko, vifungo vya nje na kazi za kuhudumia jamii

Katika ziara hiyo bw. Mpanju ameambatana na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Dkt.Edson Makallo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi na wilaya za Nachingwea, Ruangwa na Lindi, Kamanda wa Magereza mkoa wa Lindi na wilaya hizo tatu, Mahakama, wapelelezi na waendesha mashtaka mkoa wa Lindi.