Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

NATIONAL PROSECUTIONS SERVICES

DPP MWAKITALU ATEMBELEA NA KUKAGUA HALI YA MAGEREZA UKONGA NA KEKO JIJINI DAR ES SALAAM
12 Jun, 2021
DPP MWAKITALU ATEMBELEA NA KUKAGUA HALI YA MAGEREZA UKONGA NA KEKO JIJINI DAR ES SALAAM

Na Rebeca Kwandu Ofisi ya Taifa ya Mashtaka

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Sylvester Mwakitalu amefanya ziara ya ukaguzi katika Magereza ya Keko na Gereza Kuu Ukonga ya jijini Dar es Salaam ili kujionea hali halisi ya magereza hayo, kuzugumza na mahabusu pamoja na wafungwa na kuahidi kushirikiana na vyombo vingine kutatua changamoto zinapelekea kuwepo kwa msongamano ndani ya magereza hayo.

Akizungumza mara baada ya kuhitimisha ziara hiyo aliyoongozana na baadhi ya watendaji kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu na Mkoa wa Dar es Salaam , Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Mwakitalu amesema lengo la ziara hiyo ni kujionea hali halisi ya magereza, kuwasikiliza mahabusu na wafungwa ili kubaini changamoto mbalimbali zinazowakabili mahabusu na wafungwa kufuatia kesi mbalimbali zilizoko mahakamani.

“Ujio wangu hapa ni kwa ajili ya kujionea hali halisi ya msongamano pamoja na kusikiliza kero za mahabasu, wafungwa na magereza kwa ujumla ili niweze kufanyia kazi maeneo yale yanayohusu ofisi yangu “Alisema DPP Mwakitalu.

Mkurugenzi Mwakitalu amesema Magereza mengi nchini yanakabiliwa na msongamano mkubwa wa wafungwa na mahabusu kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa hali ya uhalifu nchini.

Aidha, Mkurugenzi Mwakitalu amewataka watanzania kuacha kujihusisha na uhalifu hali ambayo inachangia kuongezeka kwa msongamano magerezani huku akiahidi kufanya kazi kwa nguvu na bidii ili mashauri yaweze kusikilizwa kwa haraka na wakati.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi wa Mashtaka ametembelea na kujionea uzalishaji mkubwa wa Bidhaa (Fanicha) zinazotengenezwa na wafungwa katika gereza kuu Ukonga

Ziara hiyo ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini imelenga katika kusikiliza, kupokea malalamiko na changamoto mbalimbali zinazohusiana na masuala ya mashtaka ili ofisi yake iweze kuyatafutia ufumbuzi ili kupunguza changamoto na msongamano magerezani.

Katika ziara hiyo Mkurugenzi wa Mashtaka ameambatana na Mkurugenzi wa Divisheni ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi Bw. Oswald Tibabyekomya, Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Dar es Salaam Bi. Mkunde Mshanga na Wakuu wa Mashtaka Wilaya zote za Dar es Salaam.